“Sala ni mazoezi ya kila siku yanayotupa nguvu rohoni na kutujengea mahusiano mema na Mungu. Sali wakati unapofanikiwa, sali ukiwa na furaha, sali ukiwa na amani, sali hata usipohitaji sala. Sala ni hazina yako ya baadaye wakati usioujua wewe. “Salini kila wakati.” (1Thesalonike 5:17)
Sali uamkapo, sali uwapo safarini, sali uwapo kazini, sali ulalapo. Usiache kusali hata kama hujapata majibu ya shida yako, bado uko kwenye foleni wenda kesho Mungu atapokea maombi yako. Sali ukiamini kuwa Mungu ni mwaminifu anasikia maombi ya watoto wake, wanaomuomba pasipo kukata tamaa.
“Sala yake mnyenyekevu hupenya mawingu, wala haitatulia hata itakapowasili; na dua yake itafika hima mbinguni. Wala haitaondoka hata Aliye juu atakapoiangalia, akaamua kwa adili, akatekeleza hukumu.” (Yoshua bin Sira 35:17-18)
Sala
ni kama mto unaotiririsha maji ukisali kwa imani Mungu atatiririsha mito ya baraka juu yako. Unapofanikiwa kumbuka kumshukuru Mwenyezi Mungu. Usimsahau
Mungu aliyekuvusha salama katika magumu yote, kwani mbele ya safari yako bado
kuna magumu mengi. Usimsahau Mungu aliyekusaidia jana, kwani kesho utahitaji tena
msaada wake. Usisahau wema wa Mungu aliokutendea maishani mwako, sali daima
umshukuru na kumuomba asiziondoe fadhili zake kwako.
"Nitakushukuru Mungu kwa moyo wangu wote; nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu. Nitafurahi na kushangilia kwa sababu yako; nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mkuu."( Zaburi 9:1-2)