Vijana wategemewa,
ndilo la kesho Taifa.
Uwepo wenu vijana,
ni furaha kwa Taifa.
Wa kesho viongozi wetu,
ni ninyi vijana wetu.
Tambua thamani yenu,
tunu ya taifa letu.
Msipeperushwe vijana,
na upepo naopita.
Jifunze kujisimamia,
maisha kuyaongoza.
Usiishi kama ndege,
kijana jitegemee.
Fanya kazi kwa bidii,
Mungu tawajalieni.
Jiepushe na makundi,
yasiyo na maadili.
Kwani takupotosheni,
maisha vurugieni.
Yajenge maisha yako,
kingali kijana bado.
Weka sahihi malengo,
yawe ndiyo dira yako.
Uchaguzi ni wa kwako,
kunyoa au kusuka.
Chagua lililo jema,
likufae maishani.
Fanya kazi kwa bidii,
jitume kila wakati.
Uvivu uepukeni,
sijebaki masikini.
Imani yenu kwa Mungu,
daima lindeni vema.
Kumuomba msichoke,
tawajibu kwa wakati.
Heshimu wazazi wenu,
na wote walowalea.
Baraka mtapokea,
kutoka kwake Muumba.
Mwisho tunawaombea,
nguvu kazi ya taifa.
Mungu awalinde vema,
pia awafanikishe.
Muwe vijana hodari,
wapenda maendeleo.
Mkijibidisha vema,
taifa letu kulijenga.

“Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu. Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.” 1 Yohana 2:14–17